Dar es Salaam/Dodoma. Bunge
la Katiba linaloendelea mjini Dodoma kwa sasa liko katika hatihati ya kuendelea
baada ya kufunguliwa kesi ya kuhoji madaraka yake.
Kesi hiyo ilifunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam jana na Mwandishi wa Habari Saidi Kubenea, kupitia kwa wakili wake Peter
Kibatala, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Katika kesi hiyo iliyopewa usajili wa namba 28
ya mwaka 2014, Kubenea anaiomba mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya Mamlaka ya
Bunge la Katiba. Kubenea amefungua kesi hiyo akiomba mahakama itoe tafsiri
hiyo, chini ya vifungu vya 25 (1) na 25 (2) vya Sheria ya Marekebisho ya
Katiba namba Namba 83 ya mwaka 2011.
Sambamba na kesi hiyo ya kuomba tafsiri ya mamlaka
ya Bunge hilo, pia Kubenea amewasilisha maombi mahakamani hapo akiiomba
mahakama itoe zuio la muda la kusimamisha Bunge hilo ili kusubiri uamuzi wa
maombi ya tafsiri hiyo.
Maombi hayo ya kusimamisha Bunge hilo kwa muda
yaliyopewa usajili wa namba 29 ya mwaka 2014, pamoja na maombi ya msingi ya
tafsiri ya mamlaka ya Bunge yote yalifunguliwa mahakamani hapo jana chini ya
Hati ya Dharura.
Katika kesi hiyo ya msingi anaiomba Mahakama hiyo
itoe tafsiri sahihi ya masharti ya vifungu hivyo vya sheria hiyo na pia itamke
kama Bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha maudhui ya Rasimu ya Katiba
iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa kiwango gani.
Kwa mujibu wa hati ya madai, Kubenea anadai kuwa
msingi wa kesi hiyo unatokana na uamuzi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania wa Desemba Mosi, 2011, lililopitisha Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba. Anasema sheria hiyo ilikuwa na lengo la kuratibu mchakato wa kutungwa
kwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Anaendelea kusema kuwa kutokana na sheria
hiyo, Rais aliunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na mambo mengine
vilevile kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mapendekezo ya Katiba Mpya na
kwamba kwa msingi huo Tume hiyo iliandaa Rasimu ya Katiba.
Anadai kuwa baada ya Tume hiyo kuundwa iliendelea
kukusanya maoni ya wananchi yaliyotolewa katika mikutano ya hadhara na katika
miundo tofauti ikiwamo mabaraza ya Katiba yaliyoanzishwa kila wilaya kwa lengo
hilo.
Hati hiyo inaendelea kueleza kuwa kwa mujibu wa
takwimu halisi za tume hiyo, jumla ya watu 333,537 walitoa maoni yao
katika nyanja tofauti, tofauti za mapendekezo ya Katiba, ambayo ndiyo Tume ya
Mabadiliko ya Katiba iliyatumia kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya.
Inaendelea kueleza hati hiyo kuwa baada ya Rais
kukabidhiwa rasimu ya mwisho Desemba 8, 2013, kwa mujibu wa vifungu vingine vya
sheria hiyo, aliunda Bunge la Katiba kwa lengo la kujadili Rasimu ya Katiba na
hatimaye kupata Katiba Mpya.
Hata hivyo, kwa mujibu wa hati hiyo baada ya Bunge
la Katiba kuundwa, mjadala uliibuka ndani na nje ya misingi ya
kisheria kuhusu mamlaka yake, kama Bunge linaweza kwenda kinyume na Rasimu ya
Katiba iliyowasilishwa na tume hiyo.