Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein
ametupilia mbali maombi ya kumtaka kufungua mazungumzo na viongozi wa
Ukawa, ili kupatikana kwa mwafaka kwa wabunge wa Bunge la Katiba kutoka
Zanzibar na kurejea bungeni.
Akizungumza na Mwananchi Katibu wa Kamati ya Kuwaunganisha
wabunge kutoka Zanzibar, Mohamed Yussuf Mshamba amesema kamati yake imepokea
barua maalumu kutoka Ofisi ya Rais ikiwataarifu kuwa Rais hayuko tayari
kufungua mazungumzo hayo.
“Tumepokea majibu kutoka Ofisi ya Rais, Ikulu
Zanzibar, tumeelezwa kuwa suala hilo ni vyema likabaki mikononi mwa Bunge
la Katiba na suala la usuluhishi imeshauriwa tufanye wenyewe ZIRPP,” alisema
Mshamba.
Aidha alisema kwamba kutokana na msimamo huo wa Rais Dk
Shein, kazi ya kuwaunganisha wabunge wa Zanzibar imekuwa ngumu kwa vile
matarajio ya ZIRPP ilitegemea kazi hiyo ingerahisishwa na Rais na kuzika
tofauti ya kimsimamo.
Mshamba alisema maombi yao waliyawasilisha Agosti mwaka
huu baada ya kamati ya kuwaunganisha Wazanzibari kukamilisha kazi ya
kukusanya maoni ya wananchi kupitia kongamano la wazi juu ya nini
kifanyike na kuhakikiisha Wazanzibari wanamaliza tofauti zao na kutetea
maslahi ya Zanzibar.
‘Kwa ufupi kazi ambayo tumekuwa tukijaribu kuifanya imekuwa
ngumu, tunachowaomba wabunge wa Zanzibar waache tofauti za kiitikadi na kuweka
mbele maslahi ya Zanzibar, njia pekee rahisi na mwafaka warudi bungeni
kushirikivikao,” alisisitiza Mshamba.
Alisema kimsingi kuna makosa yaliyofanyika tokea mwanzo,
ikiwa ni pamoja na utungaji wa sheria yenyewe ya Bunge la Katiba na kujikuta
wakiingizwa wanasiasa kwenye Bunge hilo, badala ya kuwa la wataalamu na watu
wengine wasiotokana na vyama vya kisiasa.
Mshamba alieleza kuwa kuanza kwa ‘mguu’ huo mbaya kumesababisha
kuzuka kwa mivutano na mijadala yenye mitazamozaidi ya itikadi za kisiasa
badala ya kuongozwa na nguvu ya hoja, ufahamu, upembuzi yakinifu na uzoefu wa
wabunge wa Bunge hilo.
“Chadema pekee ndicho ambacho katika ilani yake iliahidi kuwa
kikishika madaraka ya uongozi kitabeba jukumu la kuandika katiba mpya, si
CCM, NCCR-Mageuzi, TLP wala CUF vilivyoahidi jambo hilo, sasa
inashangaza kuona vyama hivyo vimekuwa mstari wa mbele kushupalia Katiba
Mpya na kususia Bunge la Katiba,” alisema Mshamba.