Dar es Salaam. Jumuiya
ya Kikristo Tanzania (CCT) imetoa tamko zito ikieleza kushangazwa na kauli ya
Rais Jakaya Kikwete ya kupinga mapendekezo yaliyomo katika Rasimu ya Katiba
iliyotokana na maoni ya Watanzania na kusema kitendo hicho kimeishusha hadhi Tume
ya Mabadiliko ya Katiba aliyoiteua.........
Tamko hilo la CCT ni
mwendelezo wa lawama ambazo Rais Kikwete amekuwa akitupiwa na taasisi na watu
mbalimbali kutokana na mchakato wa kuandika Katiba Mpya kwenda mrama baada ya
mkuu huyo wa nchi kueleza maoni yake dhidi ya mapendekezo ya muundo wa Serikali
ya Muungano wakati akilihutubia Bunge la Katiba.
Miongoni mwa watu
waliojitokeza kuzungumzia kauli hiyo katika siku za karibuni ni aliyekuwa
Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, maaskofu wa Kanisa Katoliki, katibu
mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif
Sharrif Hamad.
Jana, CCT iligongomea
msumari juu ya lawama hizo ikifananisha kauli ya kiongozi huyo aliyoitoa Machi
21, mwaka huu wakati akifungua Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma na mama
anayeamua kubeba mimba na kujifungua kwa uchungu, kisha kumtelekeza mtoto,
badala ya kumfurahia.
Pia katika tamko lake
(limechapishwa kwa ukamilifu Uk. 36 wa gazeti hili), jumuiya hiyo imewataka
wajumbe wa Bunge hilo kuheshimu maoni ya Watanzania yaliyomo katika Rasimu ya
Katiba na kuacha kujadili maoni ya vyama vyao vya siasa.
“Inashangaza jinsi
chama kimoja cha siasa kinavyolazimisha wabunge na wanachama wake kukubaliana
na mapendekezo yake ambayo yanapingana wazi na yaliyomo katika rasimu ya
Katiba,” linaeleza tamko hilo lililotolewa baada ya Mkutano wa 48 wa
Halmashauri Kuu ya Jumuiya hiyo uliofanyika Julai 2 na 3 mjini Dodoma.
Tamko hilo pia limetaja
mambo mengine saba yanayolikabili Taifa.
Kabla ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba kutoa rasimu
ya pili ya Katiba Desemba 30, CCM ilisambaza waraka kuwaarifu wajumbe wa Bunge
la Katiba kutoka CCM kuwa msimamo wa chama hicho tawala ni Muungano wa serikali
mbili, tofauti na mapendekezo ya wananchi yaliyo kwenye rasimu hiyo ambayo
yanataka serikali tatu.
Licha ya mara kadhaa
Jaji Warioba kutetea kile kilichopendekezwa na Tume yake, wajumbe hao kutoka
CCM wameyapinga maoni hayo na kusisitiza kuwa yanaweza kubadilishwa kadri Bunge
la Katiba litakavyoona inafaa.
Kitendo hicho
kilisababisha wajumbe kutoka vyama vingine kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), ambao Aprili 16 uliamua kususia vikao vya Bunge hilo ukitoa masharti
kuwa utarejea bungeni kama chombo hicho cha kuandika Katiba kitajikita kujadili
mapendekezo ya wananchi kama yalivyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba.
Bunge hilo litaendelea
na vikao vyake Agosti 5 na mwenyekiti wake, Samuel Sitta anahaha kushawishi
Ukawa walegeze msimamo wao.
Katika hotuba yake ya
kufungua Bunge la Katiba, Rais Kikwete aligusia mambo kadhaa yaliyomo katika
Rasimu ya Katiba na kutaka yatazamwe kwa kina, huku akibainisha kuwa mengine
hayawezekani kutekelezeka, ikiwa ni pamoja na muundo wa serikali tatu kwa
maelezo kuwa idadi ya watu waliotaka muundo huo ni ndog