Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba wamegawanyika
vipande viwili. Kipande kimoja kiko Dodoma kikiendelea na mchakato wa kujadili
upatikanaji wa Katiba mpya.
Kipande kingine cha wajumbe wanaounda Bunge hilo
maalum kimeendelea na na msimamo wake wa kugomea mjadala wa Bunge Maalumu la
Katiba hadi watakapokubali kuheshimu maoni ya wananchi yaliyomo katika Rasimu
ya Tume ya Jaji Warioba.
Kipengele kinacholeta mzozo ni muundo wa serikali
ambapo kundi linaloundwa na upande wa CCM linasimamia kwenye muundo wa muungano
wa serikali mbili badala ya tatu zilizo katika rasimu hiyo.
Watu wa kada mbalimbali wakiwemo viongozi wa
madhehebu mbalimbali ya dini wametoa ushauri wao kwa wajumbe wa Bunge hilo
maalumu la Katiba wakiwataka kutumia busara zaidi badala ya nguvu katika
kutekeleza jukumu hilo lililopo mbele yao.
Mbali na viongozi wa vyama vya siasa, wasomi,
wanasiasa na wananchi wa kawaida vile vile wamekuwa na maoni, ushauri na maombi
yao kwa wajumbe hao kurejea misimamo yao na kutazama mzigo waliopewa na
wananchi
Wakati Bunge likiendelea watu wa kada mbalimbali,
wasomi kwa wasiosoma, wafanyakazi, wafanyabiashara na wakulima, wote kwa ujumla
wao neno lao ni moja kuwa watanzania wanataka Katiba itakayotokana na maoni na
mapendekezo yao waliyoyatoa katika Tume ya warioba.
Ujumbe huo wa watanzania umeelekezwa moja kwa moja
kwa makundi yote mawili yanayounda Bunge maalum, lile linalounda Ukawa na lile
linalobebwa na Chama tawala CCM.
Watanzania walio wengi wanayatazama makundi yote
mawili lile la Ukawa na lile la Tanzania kwanza (CCM) yanayounda Bunge maalumu
la Katiba kama yenye ubinafsi na yaliyosahau jukumu walilopewa na wananchi, la
kuwapatia Katiba mpya.
Kwamba makundi hayo yamewaweka kando
wanaowawakilisha na kuamua kujiwakilisha wenyewe na vyama vyao. Kwamba mchakato
unavyoonekana sasa ni kuwa umetekwa na wanasiasa kila kimoja kikilenga
kujinufaisha.
Wachambuzi wa masuala ya siasa na Katiba wanasema
kinachoonekana kukwamisha mchakato wa kupatikana kwa Katiba mpya ni ubinafsi wa
wanasiasa na kwamba kinachopaswa kufanyika ni kwa wanasiasa wote waliopo ndani
ya Bunge hilo maalumu kujivua uanasiasa wao na kubaki na Utanzania.
Kwamba wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba waweke
pembeni upenzi, ushabiki na ukereketwa wa yale makundi yaliyowapeleka bungeni
na kubakiza utanzania na uwakilishi wa wananchi.
Buberwa Kaiza, Mchambuzi wa masuala ya siasa na
utawala bora nchini, anasema, wajumbe wa bunge maalumu wanapaswa watambue jambo
moja kuwa wanawawakilisha wananchi na sio kujiwakilisha wenyewe au vyama vyao.
source mwananchi.