Zanzibar. Madai ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuingia katika
kinyang’anyiro cha urais yameibua mjadala mkali kutoka kwa baadhi ya wanasiasa,
wasomi na wananchi wa Zanzibar ambao wamesema hafai kutokana na kauli yake kuwa
‘Zanzibar si nchi’.
Wakizungumzia uamuzi huo ulioripotiwa na vyombo vya habari juzi,
baadhi ya wananchi hao wamempinga na wengine kumuunga mkono.
Aliyekuwa mgombea mwenza wa TLP katika Uchaguzi Mkuu 2010,
Abdallah Othman Mgaza alisema Pinda anaponzwa na kauli yake kuwa Zanzibar si
nchi... “Zanzibar ni nchi kamili ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa
kutojua kwake akasema si nchi na kuwakera Wazanzibari. Anapoteza muda wake bure
kwa kufikiria urais wa Muungano, sehemu moja ya dola hawana imani naye.”
Mwanasiasa mkongwe Zanzibar, Soud Mwana Nassor (74) alisema
katika uchaguzi ujao, Watanzania wanahitaji rais awe kiongozi mwenye sauti
itakayosikilizwa na wananchi, mwenye uwezo wa kusimamia uamuzi wake na asiwe na
makundi wala upendeleo katika uendeshaji wa Serikali.
“Napata taabu kusikia majina yanayotajwa hivi sasa ya wanaotaka
urais, hata zile mamlaka walizokabidhiwa wazisimamie zimewashinda,” alisema
Soud ambaye aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa UDP Zanzibar.
Mkurugenzi wa Uenezi, Habari na Mawasiliano kwa Umma wa CUF,
Salum Abdallah Bimani alisema chama hicho kimepata mshangao kusikia Pinda
akitaka kuwamo katika orodha ya wanaojitaja kuwania urais wa Muungano wakati
upande mmoja wa Muungano bado una kinyongo naye kwa matamshi yake yaliyodai
Zanzibar si nchi.
“Ndugu zetu CCM Zanzibar wana kawaida ya kutotusikiliza na
kutubeza, kwa hili tunawaomba chondechonde wafungue masikio yao, akiwa waziri
mkuu alisema Zanzibar si nchi, akipata urais ataitangaza nchi yetu mkoa na
kutuletea gavana mkaazi,” alisema Bimani.
Hata hivyo, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM, Wilaya ya Mjini,
Baraka Mohamed Shamte alisema kitendo cha Pinda kujitokeza mapema ni mwafaka na
kitasaidia watu kumpima, kumchambua na kuainisha sifa zake kabla ya kuchukua
fomu na taratibu za vikao vya CCM kufanyika.
“Tanganyika na Zanzibar ziliungana na kupata dola moja, nje ya
nchi Zanzibar si nchi, ndiyo maana hata katika kesi ya uhaini iliyowakabili
wanachama 18 wa CUF Mahakama ilitamka Zanzibar si nchi na hakuwezi kufanyika
uhaini,” alisema Shamte.
Alisema wanaomponda Pinda kwamba ni dhaifu wanashindwa kuelewa
kama yeye ni waziri mkuu chini ya Rais anayetawala dola na si mwamuzi wa mwisho
katika usimamizi wa masuala ya kiutawala.
Mwanasheria, Omar Makame alisema suala la Pinda kutaka urais wa
Muungano litaamuliwa na wakati ingawa wanasiasa wengi wanaotajwa kuwania nafasi
hiyo bado hawajawekeza na kukubalika ipasavyo upande wa pili wa Zanzibar.
source Mwananchi;