Jeshi la Polisi limelazimika kutumia
nguvu ikiwamo kupiga risasi za moto hewani ili kutuliza vurugu zilizoibuka
katika eneo la mkutano ulioitishwa na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter
Msigwa.
Katika mkutano huo, mbunge huyo alikuwa na lengo la kuzungumza
na waendesha pikipiki maarufu bodaboda pamoja na kusikiliza kero zao.
Hata hivyo, wakati Mchungaji Msigwa akiwa ameitisha mkutano huo,
Mwenyekiti wa Chama cha Madereva Bodaboda (CMB) Manispaa ya Iringa, Joseph
Mwambopa aliitisha mwingine kwa wanachama wake muda huo huo katika Viwanja vya
Mwembetogwa.
Hali hiyo ilielezwa kama njia ya kuleta vurugu ingawa waendesha
bodaboda wengi walihudhuria mkutano ulioandaliwa na mbunge huku idadi ndogo
ikihudhuria kwa Mwambopa aliyekuwa na msimamo tofauti.
Kuanza kwa vurugu
Vurugu hizo zilianza muda mfupi baada ya Mwambopa na watu
waliokuwa wakimuunga mkono kuwasili katika mkutano wa Mchungaji Msigwa na
kushinikiza kuingia kwa nguvu.
Baadhi ya washiriki walipinga hatua ya kiongozi huyo wa
waendesha bodaboda kuingia kwa madai kwamba hawamtaki kutokana na kitendo chake
cha kuwakataza wanachama wake kutoshiriki mkutano huo.
Hatua hiyo iliibua mzozo na kusukumana jambo lililosababisha
polisi kufika eneo hilo na kupiga risasi za moto hewani ili kutuliza ghasia na
hatimaye kumkamata Mwambopa na kuondoka naye.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Msigwa aliwataka vijana wakiwamo
waendesha bodaboda kuepuka kutumiwa na wanasiasa kama daraja la kufikia malengo
yao. “Uongozi ni zaidi ya misaada, kiongozi anapaswa kuwaonyesha watu njia ya
kufikia mafanikio,”alisema Msigwa.
Pia aliwashauri waendesha bodaboda kuanzisha chama kingine kama
wanaona kuna sababu ya kufanya hivyo.
source Mwananchi;
source Mwananchi;