Rais Jakaya Kikwete amemwagiza Waziri wa
Maji, Profesa Jumanne Maghembe kwenda kuwaeleza wananchi wa Mji wa Dumila
wilayani Kilosa sababu za kusuasua kwa utekelezaji wa mradi wa maji na lini
tatizo la kukosekana kwa huduma hiyo litapatiwa ufumbuzi.
Pia ametoa agizo kama hilo kwa watendaji wa Kitengo cha Maafa
katika Ofisi ya Waziri Mkuu, ambao kwa upande wao, wametakiwa kuwaeleza
walioathiriwa na mafuriko yaliyotokea mapema mwaka huu, kiini cha kasi ndogo ya
ujenzi wa makazi yao.
Rais Kikwete alitoa maagizo hayo juzi usiku alipokuwa
akizungumza na wananchi wa Dumila baada ya kufungua barabara mpya ya
Dumila-Ludewa wilayani Kilosa, yenye urefu wa kilometa 45 iliyojengwa kwa
Sh48.69 bilioni.
Alisema tatizo la maji katika mji huo ni la muda mrefu na kwamba
inashangaza kusikia kuwa hata utekelezaji wa mradi ambao ungemaliza kero hiyo
kwa wananchi, umekuwa wa kusuasua kwa sababu ambazo hazijulikani.
Kwa sasa sehemu kubwa ya wananchi wa mji huo ulioko katika
Barabara Kuu ya Morogoro- Dodoma, wanategemea zaidi maji ya kununua
yanayopatikana kutoka katika vyanzo visivyokuwa vya uhakika.
Kwa mujibu wa baadhi ya wananchi, dumu moja la maji hayo,
linauzwa Sh500.
“Mwaka 1993 nikiwa waziri nilifanya mkutano hapa (Dumila) wakati
huo Mbunge wa Kilosa alikuwa marehemu Shaweji (Abdallah), mtu mmoja alisimama
na kumtaka mbunge aeleze kwa nini tatizo la maji halipatiwi ufumbuzi.
“Najua hizo zilikuwa ni hasira, lakini fikiria nimekuwa waziri
hadi sasa nimekuwa Rais, tatizo bado lipo. Sasa nasema hivi, namwagiza Waziri
wa Maji achague ama Jumamosi au Jumapili ya wiki ijayo, aje hapa awaelezeni
lini tatizo hili litakwisha. Haiwezekani niondoke madarakani kabla tatizo la
maji Dumila halijapatiwa ufumbuzi,” alisema Rais Kikwete.
Pia alielezea kutoridhishwa kwake na kasi ndogo ya ujenzi wa
makazi ya watu waliokumbwa na mafuriko na kwamba hatua lazima zichukuliwe
kuharakisha ujenzi wa makazi hayo ili wananchi hao waweze kuishi maisha ya
kawaida.
“Nawaagiza watendaji wa Kitengo cha Maafa katika Ofisi ya Waziri
Mkuu, nao waje waseme kwa nini kasi ya ujenzi wa makazi ya watu walioathiriwa
na mafuriko ni ndogo,” alisema.
Kuhusu barabara aliyoifungua, Rais Kikwete alisema itakuwa
kichocheo kikubwa cha maendeleo ya wananchi wa Dumila na maeneo mengine ya
jirani.
“Shabaha yetu ni kuona kuwa barabara hii inatoka hapa
Dumila-Ludewa-Kilosa hadi Mkata ili kuchochea kasi ya maendeleo,” alisema na
kumpongeza Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli kwa ujenzi wa barabara nchini.
source Mwananchi;
source Mwananchi;