Dar es Salaam. Malkia wa muziki wa R&B, Lady Jay Dee amedai
kuwa maadui zake wamebuni njia mpya ya kumwangusha, baada ya zile za awali
kutofanikiwa.
Katika waraka mrefu aliouandika katika mtandao wa facebook, Lady
Jay Dee alisema watu wasiopenda mafanikio yake wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali
kumwangusha, lakini hata hivyo wameshindwa.
Jay Dee analalamikia habari iliyoandikwa juu yake kuwa amekuwa
katika uhusiano mpya na kijana aliyemzidi umri, jambo analosema halina ukweli.
Habari hiyo inahusishwa na kile kilichodaiwa kuwa mwanamuziki
huyo ameachana na mume wake, Gadner G Habash, ambaye ni mtangazaji wa kituo cha
redio Times FM.
Jide ameandika: “Hata kama nimeachana na mume wangu, siyo sababu
ya kunihusisha katika uhusiano na mwanamume mwingine yeyote. Habari hii
imenivunjia heshima. Nafikiri lengo la uzushi huu ni kumfanya Lady Jaydee
aonekane mtu asiyefaa.”
Habari hiyo ilipambwa na picha ambazo alizipiga mwenyewe kwa
kutumia simu ya mume wake.
Aliongeza: “Ni vizuri kuzusha vitu ambavyo angalau unavijua,
hizi picha zilipigwa kwa simu ya Gadner ambaye mnasema nimeachana naye, hamuoni
kama mnawadanganya watu?”
Aliongeza kuwa huenda aliyeanzisha habari hizo ameona zile
ambazo zilikuwa zikivuma wakati fulani, zimeshuka chati.
Alihoji: “Je, wimbo Jay Dee mgumba, Jay Dee tasa umeshuka chati
ndiyo maana mmeamua kuleta mwingine?”
Hata hivyo, alisema lengo la
wanaoanzisha uzushi juu yake ni kumdhoofisha lakini anaamini jinsi alivyoshinda
vita ya kwanza, atashinda tena vita ya pili. “Hata kama ndoa yangu haiko sawa,
niacheni.
Lakini isiwe sababu ya kuendelea kunichafua kwa maneno ya
kizushi. Siyo lazima niandikwe, kwa sababu nilikuwapo kabla ya kuandikwa
sana... nitaendelea kuwapo bila kuandikwa.”