Wakati Serikali ikihimiza tohara ya mwanamume kama mbinu mojawapo
mahususi ya kujikinga na maambukizi ya Ukimwi, bado zipo imani potofu
zinazokinzana na juhudi hizo.
Matangazo ya redioni na kwenye mabango yanasema wazi kuwa
mwanamume aliyetahiriwa anapunguza kwa asilimia 60 uwezekano wa kuambukizwa
Virusi vya Ukimwi iwapo atafanya mapenzi na mwenzi mwenye virusi.
Kwa upande mwingine jamii ambako kampeni za tohara zinaendelea,
kwa mfano jamii zilizoko mkoani Shinyanga zinao watu wanaoamini kuwa tohara ya
mwanamume ni ‘suala la waswahili’. ‘Waswahili’ mkoani humo humaanisha waumini
wa madhembu ya Kiislam.
Imani kama hizi haziji bila sababu. Ni kweli kwamba waumini wa
dini ya Kiislam na wale wanaojiunga na madhehebu hayo, wanashauriwa kufanya
tohara ya mwanamume kama mojawapo ya sharti muhimu.
Ukweli ni kuwa tohara ni jambo jema, liwe kwa ajili ya sababu za
kiimani ama za kiafya tu. Hata vitabu vya kikristo, hasa Biblia Takatifu,
inashauri wanaume kutahiriwa siku ya nane tu tangu kuzaliwa.
Wapo pia wanaoamini kuwa wanaume wenye umri mkubwa hawafai
kufanyiwa tohara.
“Kweli kabla ya kuja kwenye sehemu ya tohara nilifikiri sana
kwamba inawezekanaje kupona kidonda mimi mtu mzima hivi?” anahoji Denis Mabala,
mkazi wa Nyankende, Kahama.
Wasiwasi wake ulimfanya awatangulize kwanza watoto wake ili
kuona iwapo kweli vidonda vinavyotokana na operesheni ya tohara vinapona
haraka.
“Baadaye nilifahamu kuwa walikuwapo hata walionizidi umri ambao
walitahiriwa hivi karibuni na baada ya siku chache walirudia kufanya kazi zao,
basi ndiyo nikaamua na mimi kwenda kutahiriwa,” anaongeza Mabala, huku
akitabasamu.
Takwimu Wilaya ya Kahama
Kwa mujibu wa meneja wa huduma ya tohara ya mwanamume wa
Hospitali ya Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, Masaga Odhiambo, takwimu
zinaonyesha wazi kuwa miongoni mwa wanaume wa rika lengwa (miaka 10-49) ni wale
wa umri wa chini ndiyo hujitokeza zaidi.
Anasema wanaume wenye umri wa miaka 15-24, 652 wamejitokeza
kufanyiwa tohara katika Kituo cha Hospitali ya Kahama, wakati wale wa umri wa
miaka 25-34 wamejitokeza 113 tu tangu Januari mwaka huu.