Dar es Salaam. Sakata la waraka wa Mkakati wa Mabadiliko
uliosababisha kuvuliwa vyeo ndani ya Chadema kwa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu,
Zitto Kabwe limeibuka kwa sura mpya, safari hii likimkwamisha Ofisa wa Sera na
Utafiti wa chama hicho makao makuu, Mwita Waitara kuwania uongozi
.
Waitara amekumbana na kigingi hicho hivi karibuni katika
uchaguzi wa chama hicho Mkoa wa Mara baada ya kuwekewa pingamizi na jina lake
kuondolewa katika orodha ya wagombea uenyekiti wa mkoa kwa tuhuma za kuhusika
kuandaa waraka huo.
Waraka huo ambao ulisababisha pia viongozi wawili, aliyekuwa
Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati
Kuu, Profesa Kitila Mkumbo kufukuzwa uanachama, ulieleza kuwa kuna kiongozi
mwingine waliyeshirikiana naye aliyetajwa kama M2, kuwa alikuwa amebaki makao
makuu ya Chadema.
Baada ya Zitto kuvuliwa nyadhifa zake zote kutokana na waraka
huo, alikwenda mahakamani kuzuia hatua zaidi dhidi yake na iliwahi kuelezwa na
baadhi ya viongozi wa chama hicho kuwa uanachama wake umeshikiliwa na Mahakama.
Uchaguzi huo wa mwenyekiti wa Mara ulitakiwa kufanyika Agosti
27, mwaka huu lakini kutokana na jina la Waitara kuenguliwa na kukata rufaa,
uliahirishwa ili kutoa fursa kwa makao makuu kusikiliza madai hayo.
Mwanasheria wa Kanda ya Ziwa Mashariki, Patrobas Paschal ambaye
hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa madai kwamba liko ngazi ya juu
alisema, “Tumeamua kuusitisha uchaguzi ili kutoa haki kwa pande zote kutendeka.
Kama mtu ametuhumiwa, basi apewe nafasi ya kujitetea ila kama unataka taarifa
zaidi mtafute Singo Benson (Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi
wa Kanda wa Chadema),” alisema Paschal.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Benson alisema uchaguzi huo
utafanyika baada ya uchaguzi ngazi ya Taifa kumalizika.
“Uchaguzi huo ulisimamishwa na ngazi ya kanda ambayo ndiyo yenye
mamlaka na hilo lilitokana na kuwapo kwa malalamiko, hivyo uchaguzi huo
utafanyika baada ya uchaguzi ngazi ya taifa (Septemba 14, mwaka huu),” alisema
Benson.
Waitara azungumza
Akizungumzia hatua hiyo, Waitara alisema kilichofanyika ni njama
za kutaka kumwondoa asigombee nafasi hiyo na baadhi ya wanachama na kuwa
hatakubali tuhuma hizo.
“Tuhuma hizi ni kubwa, zimenichafua, nataka huyo anayesema mimi
kuwa ni M2 nilihusika na kina Zitto aje athibitishe na atoe vielelezo,” alisema
Waitara na kuongeza:
“Sikuona sababu ya mimi kuenguliwa katika uchaguzi huo kwani
mimi sijawahi kuhojiwa na chama kuwa ndiye M2, mimi ni mfanyakazi wa makao
makuu, jambo hili limenisikitisha sana.”
source Mwananchi;