Dar es Salaam. Hatimaye Waziri Mkuu
Mstaafu Frederick Sumaye ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitajwa kuwania urais
amethibitisha rasmi kuwa atagombea kwenye uchaguzi mkuu mwakani. Kiongozi huyo
aliweka wazi nia ya kuelekea Ikulu wakati alipokuwa akihojiwa na Radio Deutsche
Welle (DW) ya Ujerumani jana mchana na hivyo kuwa kiongozi wa pili kutangaza
nia kupitia vyombo vya habari vya kimataifa.
Julai 3, mwaka huu, Naibu Waziri wa
Sayansi na Teknolojia, January Makamba alitangaza nia ya kuwania urais baada ya
kuhojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) alipokuwa amekwenda huko
kuhudhuria mkutano wa sekta ya mawasiliano.
Akifafanua kwa nini anataka kuwa rais,
January alisema kuwa huu ni wakati wa fikra mpya kushika dola na kwamba
anaamini muda wa wazee kukaa kando umefika.
Sumaye ambaye aliwahi kugusia suala hilo
kwa kusema kuwa angeweza kugombea kwenye kinyang’anyiro kijacho kama wananchi
wangetaka afanye hivyo sasa ametegua kitendawili kwa kusema kuwa yuko tayari
kuwania nafasi hiyo.
“Maana siyo kila mtu anayejaza kutaka
kwenda kugombea. Ni watu wamemtaka na wapo wengi tu ambao wanajaza kwa sababu
wametaka wenyewe eeh! Kwa hiyo kama watu wakinitaka nitagombea kwa nini
nisigombee, nitagombea na ninafikiria nitagombea,” alisema.
Hata hivyo, alionyesha kutishwa na
kiwango cha rushwa katika mchakato wa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu kwa kusema
kuwa:
“Ukweli ni kwamba matumizi ya fedha
ndiyo yamekuwa makubwa sana na kwa kiwango fulani Watanzania wanadhani, siwezi
kuwamo. Watanzania ni wale ambao wana nafasi ya kuchagua na wanadhani kama
hawajapata fedha basi huyo ambaye hajatoa fedha anaonekana kama hachaguliki.
“Ukweli ni kwamba ni jambo la hatari na
lazima tulipige vita katika nchi yetu. Matumaini yangu ni kwamba viongozi wetu
waliopo watajitahidi kupiga vita,” alisema Sumaye.
Pia kiongozi huyo alikosa baadhi ya watu
wanaosema wakati wa kuwa na rais kijana umefika kwa kusema kuwa umri hauwezi
kuwa kigezo pekee cha kumpata rais.
“Kama kuna kijana hata kama ana miaka 41
ambaye anadhani anafaa na umma unadhani anafaa si kwa sababu ni kijana hakuna
tatizo, mradi asiwe anakwenda pale kwa kusema mimi ni kijana ninayefaa. Unaweza
kusema kila kijana anafaa kuongoza hii nchi? Haiwezekani” alihoji.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
Januari 1 mwaka huu alitangaza ‘kiaina’ kuwania nafasi ya urais kwa kusema
kwamba anaanza safari ya matumaini.
Source mwananchi;