Dodoma. Kamati namba mbili ya Bunge Maalum
la Katiba imekosa theluthi mbili katika ibara 19 na 22 zinaohusiana na maadili
na miiko ya uongozi na utumishi wa umma.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Shamsi Vuai Nahodha
alisema jana katika ibara ya 19 hawakupata theluthi mbili ya kura zilizopigwa
kutoka Zanzibar.
Pia Nahodha alisema kamati yake ilikosa theluthi
mbili ya kura zilizopigwa kwa upande wa Tanzania Bara katika ibara ya 22.
Alisema katika ibara ya 19 ambayo alikosekana mtu
mmoja kutimiza theluthi mbili ya kura kwa upande wa Zanzibar.
Ibara hiyo inatamka kuwa kiongozi wa umma hatatumia
ama kutumia au kuruhusu kutumika kwa mali za umma zikiwamo zilizokodishwa kwa
Serikali kwa madhumuni ya kujipatia yeye binafsi ama kumpatia mtu mwingine
manufaa yoyote.
“Kilichofanyika katika rasimu hii kulikuwa na neno
kiongozi wa umma sasa wajumbe walio wengi wakafanya marekebisho kuwa si suala
la kiongozi tu wa umma anayepaswa kuzingatia hili hata watumishi wa umma,”
alisema.
Alisema kutokana na hoja hiyo wajumbe walio wengi
wakaongeza neno mtumishi wa umma, jambo ambalo lilikataliwa na mjumbe mmoja
kutoka Zanzibar ambaye alitaka ibara hiyo kusomeka kama ilivyo katika Rasimu ya
Katiba.
Nahodha alisema kwa upande wa ibara ya 22, wajumbe
walio wengi walitaka ibara hiyo ihamishiwe katika sura ya 11.
Ibara hiyo inahusiana na watumishi wa umma aliye
katika ajira ya kudumu hataruhusiwa kuingia katika ajira nyingine ya kudumu
yenye malipo ya mshahara.
Pia ibara hiyo inasema mtumishi wa umma atakayeamua
kugombea, kuchaguliwa na kuteuliwa kushika nafasi ya madaraka ya kisiasa ya
aina yoyote chini ya Katiba hiyo au uongozi wa ngazi yoyote katika chama cha
siasa mtumishi huyo atachukuliwa kuwa utumishi wake umekoma tangu siku ya
kuteuliwa kugombea, kuchaguliwa au kuteuliwa kushika nafasi ya madaraka ya
kisiasa au uongozi katika chama cha siasa.
Nahodha , alisema mjumbe mmoja alipinga kuhamishwa
kwa ibara hiyo katika sura ya 11 na kutaka ibakie katika sura hiyo.
Aidha, Nahodha alisema kulikuwa na mjadala wa kina
kuhusiana na ibara zinazohusiana na rushwa.
source mwananchi