Kamati hiyo inaongozwa na Naibu Waziri, Ofisi ya
Makamu wa Rais, Ummy Mwalimu na makamu wake ni Waziri wa Sayansi na Teknolojia,
Profesa Makame Mbarawa, huku ikiwa imesheheni vigogo wengine wakiongozwa na
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Viongozi wengine katika kamati hiyo ni Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uhusiano na Uratibu), William Lukuvi, Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika na Waziri wa Ulinzi na
Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi.
Wamo pia Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif
Rashid, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka na Naibu Waziri wa Maendeleo
ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana.
Jana asubuhi, Mwalimu na Profesa Mbarawa walifika mbele
ya waandishi wa habari katika Hoteli ya St Gasper wakiwa wameambatana na mmoja
wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally
Keissy.
Lengo la mwenyekiti na makamu wake lilikuwa ni
kumbana Keissy ili akanushe taarifa aliyoitoa juzi kwenye moja ya televisheni
kwamba kamati hiyo inaongoza kwa kuvunja kanuni hasa katika suala la akidi ya
vikao kutotimia.
Sinema ilivyoanza
Walipofika mbele ya waandishi wa habari, Keissy
alipewa fursa ili akanushe taarifa yake, lakini alibadili mada na kuanza
kuzungumzia masuala ya muundo wa Serikali na Bunge, huku akisema yeye ni
muumini wa serikali tatu na siyo mambo ya serikali mbili zinazopendekezwa na
wengi kutoka katika chama chake.
Kauli hiyo iliwashtua Mwalimu na Profesa Mbarawa
ambao walianza kumkatisha ili asiendelee.
“Keissy sikukuitia mambo hayo, huu ni mkutano wangu,
naomba ukanushe nilichokuitia, hayo utazungumza baadaye tafadhali sana,”
alisema Mwalimu.
Wakati huo Profesa Mbarawa na waandishi wa habari
waliokuwapo walivunjika mbavu kwa vicheko, huku yeye akiendelea kusisitiza
kwamba ni muumini wa Tanganyika.
Wakati akisema hayo, Profesa Mbarawa naye aliingilia
kati na kumtaka Keissy kueleza kilichompeleka hapo huku akimtaka aache kelele
za kupotosha wananchi kwa kuwa anachosema siyo kweli.