Dodoma. Kamati za Bunge Maalumu, zimekamilisha
kazi ya kujadili na kuchambua Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, huku ikiwa imefanyiwa mabadiliko makubwa tofauti na
ilivyokuwa awali.
Wajumbe wanatarajiwa kuanza kukutana kama Bunge zima kuanzia
Jumanne ijayo, Septemba 2, 2014 wakati kamati zitakaposoma taarifa zake baada
ya kufanya uchambuzi wa sura 15 za Rasimu ya Katiba kwa zaidi ya wiki tatu,
huku yakitarajiwa mabadiliko makubwa.
Mabadiliko yaliyofanywa yameondoa mambo makubwa yaliyokuwa
yakiifanya rasimu hiyo kuonekana mpya, hivyo sasa baadhi ya wachambuzi wa mambo
wanaiona rasimu kama ‘Katiba ya 1977 iliyofanyiwa marekebisho.’
Mwelekeo wa kubadili karibu misingi yote muhimu iliyojengwa na
tume iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba akiwa mwenyekiti, ilianza baada ya
kuwekwa kando kwa mfumo wa muungano wa Serikali tatu uliopendekezwa na badala
yake kurejea katika muundo wa sasa wa serikali mbili.
Uamuzi huo uliathiri mtiririko na muundo mzima wa sura na ibara
za rasimu hiyo, kwani sasa wajumbe wa Bunge Maalumu walilazimika kutengeneza
Katiba yenye mwelekeo wa serikali mbili na siyo tatu tena zilizokuwa
zimependekezwa na tume.
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad aliwahi kuliambia
gazeti hili kwamba mwelekeo wa uchambuzi wa rasimu kwa sura hizo 15, lazima
ufuate kile ambacho kamati zilikiamua katika uchambuzi wa awali wa sura ya
kwanza na ya sita.
Miongoni mwa mambo ambayo yameachwa baada ya kurejesha mfumo wa
serikali mbili ni muundo wa uongozi wa juu wa nchi hususan nafasi ya Makamu wa
Rais, muundo wa Bunge la Jamhuri, kupunguzwa mamlaka ya Rais, uwajibikaji na
uwajibishwaji wa wabunge na ukomo wa ubunge.
Kadhalika, habari kutoka ndani ya kamati zilisema suala la
kuwekwa kwa maadili ya uongozi kwenye Katiba nalo lilizua mjadala mkali
kutokana na baadhi ya wajumbe kutaka liondolewe kwa maelezo kwamba linapaswa
litajwe kwenye sheria na siyo Katiba.
Mambo ya muungano
Miongoni mwa mambo ambayo kuna kila dalili kwamba yatabadilika
ni Bunge Maalumu kuongeza mambo ya muungano kutoka saba yaliyopendekezwa na
tume na huenda idadi yake ikazidi 22 yaliyomo kwenye Katiba ya sasa.
Uchunguzi wa gazeti hili uliofanywa katika baadhi ya
kamati za Bunge hilo na kuthibitishwa na baadhi ya wenyeviti wake, umebaini
kuwa yapo mapendekezo ya mambo ya muungano kuongezwa, tofauti na mtazamo wa
awali kwamba yangepungua kama moja ya njia za kuondoa kero za muungano.
Tume ya Jaji Warioba ilipendekeza mambo saba tu kwenye orodha ya
muungano chini ya mfumo wa Serikali tatu, mfumo ambao hata hivyo ni dhahiri
umeshawekwa kando na Bunge Maalumu na kurejesha muundo wa serikali mbili.
SOURCE Mwananchi;
SOURCE Mwananchi;