Dodoma. Mjumbe mwingine wa Bunge la Katiba kutoka
Kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) jana alionekana kwenye Viwanja vya
Bunge na alisaini za mahudhurio.
Mjumbe aliyeonekana jana, Leticia Nyerere wa viti
maalumu, Chadema, anafanya idadi ya wajumbe waliotinga kwenye viwanja hivyo
hadi sasa kufikia watatu baada ya Chiku Abwao (viti maalumu Chadema) kuonekana
juzi na Clara Mwatuka (viti maalumu CUF) kuonekana Jumapili.
Nyerere hakuwa akihudhuria vikao baada ya Ukawa
kutangaza kususia Bunge mwezi Aprili na jana hakupatika kuzungumzia suala hilo.
Kuonekana kwa mjumbe hao kunaweza kutafsiriwa kuwa
ni kubomoka kwa ngome za Vyama vya Chadema, NCCR na CUF vinavyounda umoja huo
kwani tangu awali walikubaliana kutoshiriki shughuli za Bunge hadi pale
watakapofikia makubaliano ya hoja zao.
Msimamo wa chama hicho chini ya viongozi wao ni
kutohudhuria shughuli za Bunge Maalumu la Katiba hadi kutakapokuwa na mwafaka
wa mwenendo wa shughuli za chombo hicho, ambacho jana kiliendelea na vikao vya
kamati kujadili sura 15 za Rasimu ya Katiba.
Ukawa wanadai CCM imepora mawazo ya wananchi na
kwamba kuna mpango wa kuchakachua rasimu iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba na kuingiza mambo yenye masilahi kwa chama hicho na Serikali yake.
Vyama vinavyounda Ukawa vinadai kuwa kuzungumzia
muundo wa Muungano wa serikali mbili ni kuchakachua maoni ya wananchi ambao
walitaka muundo wa serikali tatu kama ilivyo kwenye Rasimu ya Katiba.
Bunge jana lilikutana katika kamati zake 12
zilizotawanyika katika kumbi mbalimbali kwa ajili ya kupitia sura 15 za rasimu
ya Katiba ingawa wajumbe wengine walilazimika kuanzia safari zao bungeni ili
waweze kujisajili.
Mwenyekiti wa Kamati namba tano ambayo Nyerere ni
mjumbe, Hamad Rashid Mohamed alisema mjumbe huyo hakuwa amefika katika kikao
cha jana ambacho pia kilifanyika Dodoma Hoteli.
Kuhusu mwenendo wa kikao cha kamati yake, Mohamed
alisema hadi jana mchana walikuwa wamekamilisha kupitia sura ya pili na kwamba
jioni walitarajia kuifanyia kazi sura ya tatu.
Kuhusu changamoto ya muda, Mohamed alisema: “Hiyo
ndiyo hali halisi na tukiweza tutapiga kura kupitisha ibara hizo leo (jana),
kama tukishindwa basi tutapiga kura kesho (leo) ili mradi tutumie muda ambao
upo tufanye kazi kwa ufanisi.”
source mwananchi;